Business
Biashara zadorora mjini Kilifi kufuatia likizo ya Chuo Kikuu
Wafanyibiashara mjini Kilifi kaunti ya Kilifi wanalalamikia kushuka kwa kiwango cha biashara mjini Kilifi baada ya wateja wanaowategemea kuanza likizo.
Kulingana na uchunguzi ulifanywa na Coco Fm, wafanyibiashara wengi wa nguo kuukuu mjini Kilifi wanasema kwamba uchumi wao umeshuka kwa kiwango kikubwa tangu wanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani kuenda likizo, hivyo kuathiri biashara zao.
Wakizungumza na cocofm wafanyibiashara hao wanasema kuwa uchumi wa kaunti ya kilifi huchangiwa pakubwa na idadi ya wanafunzi katika chuo hicho na wakati wanapokwenda likizoni basi biashara nyingi za mji wa Kilifi huanza kudorora.
Aidha wafanyibishara hao wametaja kupanda kwa gharama ya maisha kumechangia pia kudorora kwa biashara zao huku wakitoa wito kwa serikali kuu kuweka mikakati ya kupunguza gharama ya maisha.
“Kwa sasa matumizi ya pesa kaunti ya Kilifi imepungua yaani hakuna pesa hali ambayo inaathiri biashara kwani biashara nyingi zinategemea wanafunzi wa chuo kikuu cha pwani na kwa sasa wako likizo”, walisema wafanyibiashara hao.
Business
Bei za mafuta kuongezeka katikati ya mwezi aprili
Kenya sasa inakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta, huku mgogoro unaoendelea mashariki ya Kati ukianza kuathiri bei nchini.
Serikali sasa imeonya kuwa kufikia katikati ya mwezi Aprili, bei za mafuta huenda zikapanda ikionya kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwa sasa haliwezi kuepukika kufuatia kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.
Waziri wa hazina kuu ya kitaifa John Mbadi aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna cha kuhofia kwani wameweka mikakati kupunguza athari zake.
Ili kupunguza athari za bei za mafuta kuongezeka, serikali ilisema itatumia shilingi bilioni 17 kutoka mfuko wa ada ya uwekezaji wa mafuta kusaidia kudhibiti bei kwa mda wa miezi 3 ijayo.
Kwa sasa serikali inasema kuna akiba ya kutosha ya mafuta na shehena zaidi zinatarajiwa nchini hivi karibuni.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

