News
Wajane kaunti ya Kilifi wahimiza serikali kuangazia maslahi yao
Wajane katika kaunti ya Kilifi wamehimiza kuangaziwa kwa madhila wanayopitia katika jamii ili kuwawezesha kukidhi mahitaji yao kikamilifu.
Wajane hao walitoa wito kwa serikali kuwatambua badala ya kuwatenga kwani wamekuwa wakipitia masaibu mengi katika jamii baada ya kuwapoteza wapendwa wao.
Miongoni mwa waliyoyaweka wazi ili kuangaziwa na serikali pamoja na wadau husika ni pamoja na kupokonywa mali na wanafamilia wa waume zao, kutelekezwa na jamii, kulazimishwa kurithiwa pamoja na kuzongwa na umaskini.
Aidha walidai kwamba wamepitia manyanyaso ya kupokonywa ardhi zao sawa na kupitia wakati mgumu wanapotafuta hati miliki za ardhi walizoachiwa na waume zao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wanawake wajane kaunti ya Kilifi Elizabeth Muthoka alieleza haja ya viongozi serikalini kushirikiana na wajane ili kuangazia changamoto zao sawa na kuwasilisha hoja bungeni za kutetea maslahi yao.
“Viongozi wetu wa kile ndani ya Kilifi kaunti na Kenya nzima wakiongozwa na mama Mbeyu pale bungeni, tunataka pale ndani ya bunge la kitaifa mpeleke hoja ambayo itamuangazia mjane, ambayo mjane ataangaziwa ndani ya Katiba maana sisi hatuko mahali popote”, alisema Elizabeth.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Gavana wa Kilifi Flora Mbetsa Chibule alisema tayari serikali ya kaunti ina mikakati ya kubuni sheria ya kumlinda mjane, akiwashauri wajane kujisajili kwenye vikundi ili kunufaika na miradi ya maendeleo.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Baraza la Jamii ya Sekuye lalamikia uchimbaji wa madini kiholela
Baraza la Wazee wa jamii ya Sekuye eneo la Moyale kaunti ya Marsabit limejitokeza na kulalamikia kuharibiwa kwa mazingira ya maeneo yao hasa katika kijiji cha Dabel kutokana na uchimbaji madini kiholela.
Wazee hao wamewalaumu viongozi wao ikiwemo serikali ya kaunti kwa kulinyamazia suala hilo huku wakaazi wakiendelea kunyanyaswa raslimali zao.
Baraza hilo, chini ya Katibu wake mkuu Haji Hassan Tepo, limedai kwamba uchimbaji huo wa madini kiholela, unyakuzi wa ardhi, unyanyasaji wa jamii umechangiwa na baadhi ya wawekezaji kutoka taifa Jirani la Somalia na Ethiopia ambao hawana vibali halali.
Hassan aliimtaka serikali kupitia Waziri wa madini nchini Hassan Ali Joho kuingilia kati suala hilo na kuhakikisha uchumbaji wa madini katika kijiji cha Dabel unasitishwa kwani wawekezaji zaidi ya 20 wamebuni makundi na kuendelea kuwanyanyasa wenyeji.
Hassan aliweka wazi kwamba baraza hilo pamoja na jamii ya Sekuye linapinga mpango huo na kusisitisha kwamba hawatakubali ardhi yao wanayoitegemea kwa shughuli mbalimbali kutumika vibaya.
Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo Abdukadir Dilo alisema hali hiyo imewasabibishia hasara kwani mifugo imeangamia, uchumi wa kijiji hicho ukididimia zaidi na akamtaka rais Ruto kuingilia kati kwani licha ya Waziri Murkomen kufunga uchumbaji kufuatia utovu wa usalama bado wawekezaji kutoka Ethiopia na Somali wamekuwa wakiendeleza mpango huo.
Wazee hao hata hivyo walisisitiza kwamba hawatakubali kuachilia ardhi yao kunyakuliwa na watu wanaodai kuwa wawekezaji ilhali vijana wa eneo hilo hawana kazi, huku wanafunzi wakiacha shule na zaidi ya akina mama 22 wakiachwa na wanaume zao kufuatia suala hilo katika kijiji cha Dabel.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Murkomen ahimiza ushirikiano wa pamoja na wadau wa masuala ya ubaharia
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen, ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya washirika na wadau ili kuimarisha usalama wa baharini na maziwa makuu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano la kamati ya uongozi wa Jukwaa la ushirikiano wa taarifa ya kanda ya Indo-Pasifiki (IORIS) lililofanyika mjini Mombasa, Waziri huyo alisisitiza kuwa ushirikiano wa mapema ni muhimu katika kukabiliana na vitisho vinavyoibuka vya usalama wa baharini.
“Ushirikiano wa mapema na muhimu katika kulinda usalama wetu wa baharini,” alisema Murkomen.
Kongamano hilo la siku tatu linaandaliwa kwa pamoja na huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya (KCGS) pamoja na mradi wa njia muhimu za baharini wa Indo-Pasifiki unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU-CRIMARIO), ukiwaleta pamoja wadau wa usalama wa baharini..
Mradi wa EU-CRIMARIO umeundwa kuimarisha usalama na ulinzi wa baharini kupitia kuboreshwa kwa ushirikiano wa taarifa na uratibu wa operesheni.

Kongamano la siku tatu la kamati ya uongozi la Jukwaa la ushirikiano wa taarifa ya kanda ya Indo-Pasifiki (IORIS), Mombasa
Mpango wake mkuu, IORIS, ni jukwaa salama na lisiloegemea upande wowote linalotumia mtandao, unaounganisha zaidi ya mashirika 150 kutoka nchi 70, na kuwezesha uratibu wa operesheni za baharini kwa wakati halisi.
Kauli za Murkomen ilijiri kufuatia tangazo la Rais William Ruto kwamba kampuni ya usafiri wa baharini ya Norway, Wilhelmsen, itaajiri mabaharia 1,000 kutoka Kenya, baada ya mazungumzo na kampuni hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa EU-CRIMARIO Martin Cauchi Inglott, Mkurugenzi mkuu wa huduma ya walinzi wa Pwani ya Kenya Bruno Shioso, Naibu mkuu wa ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Kenya Ondrej Simek, pamoja na washkadau wengine.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

