News
Wajane kaunti ya Kilifi wahimiza serikali kuangazia maslahi yao
Wajane katika kaunti ya Kilifi wamehimiza kuangaziwa kwa madhila wanayopitia katika jamii ili kuwawezesha kukidhi mahitaji yao kikamilifu.
Wajane hao walitoa wito kwa serikali kuwatambua badala ya kuwatenga kwani wamekuwa wakipitia masaibu mengi katika jamii baada ya kuwapoteza wapendwa wao.
Miongoni mwa waliyoyaweka wazi ili kuangaziwa na serikali pamoja na wadau husika ni pamoja na kupokonywa mali na wanafamilia wa waume zao, kutelekezwa na jamii, kulazimishwa kurithiwa pamoja na kuzongwa na umaskini.
Aidha walidai kwamba wamepitia manyanyaso ya kupokonywa ardhi zao sawa na kupitia wakati mgumu wanapotafuta hati miliki za ardhi walizoachiwa na waume zao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wanawake wajane kaunti ya Kilifi Elizabeth Muthoka alieleza haja ya viongozi serikalini kushirikiana na wajane ili kuangazia changamoto zao sawa na kuwasilisha hoja bungeni za kutetea maslahi yao.
“Viongozi wetu wa kile ndani ya Kilifi kaunti na Kenya nzima wakiongozwa na mama Mbeyu pale bungeni, tunataka pale ndani ya bunge la kitaifa mpeleke hoja ambayo itamuangazia mjane, ambayo mjane ataangaziwa ndani ya Katiba maana sisi hatuko mahali popote”, alisema Elizabeth.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Gavana wa Kilifi Flora Mbetsa Chibule alisema tayari serikali ya kaunti ina mikakati ya kubuni sheria ya kumlinda mjane, akiwashauri wajane kujisajili kwenye vikundi ili kunufaika na miradi ya maendeleo.
Taarifa ya Joseph Jira