News
Alubbe: Wakaazi wa Pwani hawafahamu haki za ardhi
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kuangazia haki za ardhi nchini, Kenya Land Alliance KLA, Faith Alubbe amesema kuwa idadi kubwa ya wakaazi hasa wa mashinani wanakumbwa na changamoto za ardhi kufuatia ukosefu wa uelewa na ufahamu wa haki na sheria zinazofungamana na umiliki wa ardhi.
Akizungumza baada ya warsha na wanahabari mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Alubbe alikariri kuwa ardhi nyingi za wananchi zinaishia mikononi mwa mabwenyenye kutokana na wakaazi wenyewe hawana namna ya kufahamu au hata kupata elimu kuhusu masuala ya ardhi.
Kufuatia hilo Alubbe alikariri kuwa shirika hilo limeweka mikakati ya kutumia vyombo vya habari kutoa hamasa hizo kwa wananchi hali inayosababisha wao kuandaa warsha za kuwahamasisha wanahabari namna watakavyoweza kupitisha hamasa hizo kuhusu umiliki wa ardhi kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Warsha na Wanahabari mjini Malindi kaunti ya Kilifi kuhusu ufahamu wa masuala ya ardhi Pwani
“Uskwota umekithiri katika maeneo mengi humu nchini kutokana na suala kuwa hakujakuwa na mifumo hitajika ya kuangazia dhulma za kihistoria za ardhi” alisema Alubbe.
“Ni sharti jamii ipewe taarifa muhimu za jinsi ya kusajili ardhi zao kwani wanajamii wengi wanaishi kwenye ardhi ambazo hawana umiliki nazo kutokana na ukosefu wa ufahamu” aliongeza Alubbe
KLA iliandaa warsha ambayo ilijumuisha wanahabari kutoka kaunti ya Kilifi lakini pia wale wa kaunti ya Tanariver.
Taarifa ya Hamis Kombe