News
Gavana wa Isiolo Abdi Guyo atimuliwa Mamlakani
Bunge la kaunti ya Isiolo limembandua Mamlakani Gavana wa kaunti hiyo Abdi Ibrahim Guyo.
Hii ni baada ya Wawakilishi wadi 16 kati ya 18 katika bunge la kaunti hiyo kupiga kura ya kutokuwa na Imani na Gavana Guyo na kumtimua mamlakani.
Kulingana na hoja iliyowasilishwa katika bunge hilo na Mwakilishi wadi wa Sericho Abubakar Godana tangu mwezi Juni tarehe 10 ilikashifu uongozi duni wa Gavana Guyo.
Shtuma zengine zilizochangia kubanduliwa Mamlakani kwa Gavana Guyo ni pamoja na utumizi mbaya wa ofisi ya umma, ufisadi, ukiukaji wa sheria, kukwama kwa miradi muhimu ya maendeleo, kushindwa kuafikia malengo ya mapato, uteuzi wa washauri 36 na maafisa wakuu 31 licha ya kaunti hiyo kupokea mgao wa tatu wa mapato nchini miongoni mwa masuala mengine.
Hata hivyo hoja ya kumbandua mamlakani Gavana Guyo iliendelea katika bunge la kaunti hiyo licha ya Mahakaka kuu ya Isiolo kuidhinisha kusitishwa kwa hoja hiyo hadi masuala tata yatatuliwe.
Hoja ya kubanduliwa Mamlakani kwa Gavana huyo sasa imewasilishwa katika bunge la seneti kwa kuzingatia kipengele cha 181 cha Katiba ya nchi na sehemu ya 33 ya sheria za serikali za kaunti.
Kutimuliwa kwa Gavana Guyo mamlakani kuongeza idadi ya magavana waliotemwa uongozini akiwemo aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko, aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na sasa ni Gavana wa Isiolo Abdi Ibrahim Guyo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi