News
Jackson Chiwai ahukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani
Mahakama ya Kilifi imemhukumu kifungo cha miaka 15 gerezani Jackson Chiwai baada ya Mahakama kumpata na hatia ya kumnajisi mtoto mdogo wa umri wa miaka 5.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa baada ya ushahidi kamili kuwasilishwa Mahakamani.
Hakimu Obulutsa alisema kwamba hukumu hiyo imezingatia ushahidi wote uliyowasilishwa Mahakamani kiwemo ripoti ya daktari kuhusu uchunguzi wa unajisi dhidi ya mtoto huyo.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, upande wa mashtaka ukiongozwa na Kiongozi wa mashtaka ya umma katika Mahakama hiyo Ridhwan Mohammed ulieleza Mahakama kwamba mnamo tarehe 11 mwezi Mei mwaka 2024 mwendo wa saa moja jioni Jackson alimnajisi mtoto wa miaka 5 ambaye ni binamu yake.
Japo ushahidi wa mlalamishi na mashahidi wengine ambao ni watoto wenzake uliashiria kitendo hicho cha unajisi kuwa kweli baada ya watoto hao kueleza Mahakama kwamba walikuwa wakiangalia runinga chumbani wakati mama yao akiwa jikoni akipika, ambapo Jackson ambaye ni binamu yao aliingia chumbani humo na kumchukua mtoto huyo na kutoka naye nje ambapo alitekeleza kitendo hicho.
Kulingana na ushahidi wa daktari, uchunguzi na vipimo kwa mtoto huyo ilionyesha kwamba mtoto hakuwa amenajisiwa bali kulikuwa na jaribio la dhulma ya kingono kutokana na mikwaruzo kwenye uke wa mtoto huyo.
Uchunguzi wa daktari ulichangia pakubwa kwenye hukumu hiyo ambayo Hakimu Obulusta alieleza kwamba Jackson angehukumiwa kifungo cha maisha kulingana na sheria na uzito wa kesi hiyo.
Mshukiwa alihukumiwa kwa kosa mbadala la kujaribu kumnajisi mtoto huyo na kupata kifungo hicho cha miaka 15.
Mahakama hata hivyo imempa mshtakiwa siku 14 za kukata rufaa iwapo hajaridhishwa na uamuzi wa Mahakama.
Taarifa ya Teclar Yeri.