News
Joho asitisha shughuli za uchimbaji madini za kampuni ya Tata Chemials Magadi
Serikali imesitisha shughuli zote za uchimbaji madini kwa kampuni ya Tata Chemials Magadi limited kwa kukiuka sheria za uchimbaji madini.
Kwenye taarifa iliyotolewa na Waziri wa madini na uchumi wa raslimali za baharini na maziwa Ali Hassan Joho ilisema kuwa hatua hiyo inafuatia majadiliano ya miaka mingi kati ya idara ya uchimbaji madini na kampuni hiyo kuhusu wajibu wake katika kutekeleza sheria ya uchimbaji madini.
Joho alisema bado kuna masuala muhimu ya kuzingatia sheria ambayo hayajatimizwa, ikiwemo kutokuwa na mkakati wazi wa kuongeza thamani ya madini, kutolipwa kwa malipo ya mrabaha na upatanishi, ripoti zisizokamili za mauzo ya nje, utekelezaji duni wa mikataba ya maendeleo ya Jamii, ukosefu wa ajira na mianya iliyoko katika utunzaji wa mazingira.
Waziri Joho, aliamuru kampuni hiyo kuwasilisha ushahidi wa kuzingatia sheria zote kikamilifu na kulipa madeni yoyote yaliyosalia kabla ya shughuli za uchimbaji madini kuanza tena.
Taarifa ya Janet Mumbi