News

Jopo la kushughulikia fidia kwa waathiriwa wa maandamano laanza kazi

Published

on

Jopo lililoundwa na Rais William Ruto kushughulikia masuala ya fidia ya waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maadamano limeanza kikao cha wiki moja huku mjadala kuhusu uhalali na uwazi wa jopo hili ukitiliwa shaka na kupokea upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu na viongozi wa upinzani.

Jopo hilo linaongozwa na Prof. Makau Mutua na naibu wake Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK), Faith Odhiambo, ambaye uteuzi wake umeibua mjadala mkali.

Baadhi ya Wanasheria walimshutumu Odhiambo kwa “kusaliti haki,” lakini yeye alisisitiza kwamba jukumu lake ni kuhakikisha waathiriwa wa ukatili wa polisi wanapata haki waliyoikosa kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa jopo hilo lina nafasi ya kuleta mabadiliko ya kihistoria katika upatikanaji wa fidia kwa waathiriwa.

Kwa mujibu wa maelezo yake, jopo hilo si tume ya kikatiba wala chombo cha kisheria chini ya Katiba, bali ni jopo la ushauri lililoanzishwa na Rais chini ya Kifungu cha 132(4)(a).

Vile vile alibainisha kuwa wanachama wa jopo hilo si maafisa wa umma hivyo uteuzi wao hauhitaji mchakato wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Kifungu cha 260 cha Katiba.

Jopo lililoundwa na Rais William Ruto kushughulikia ya fidia ya waathiriwa wa maadamano

Hata hivyo, wakosoaji walisema linaweza kukiuka mamlaka ya ofisi huru kama Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR). Jopo hilo limekanusha madai hayo, likisema jukumu lake ni kusaidia na sio kuchukua nafasi ya taasisi zilizopo.

Wapo pia wanaouliza uhalali wa serikali kuwalipa fidia waathiriwa ilhali serikali hiyo hiyo imeshtumiwa kwa mauaji, kutoweka kwa baadhi ya wakosoaji wa serikali kwa njia tatanishi na kuacha familia na majeraha yasiyotibika.

Jopo hilo pia linasisitiza kikatiba, serikali ndiyo chombo kinachobeba wajibu wa kurekebisha madhila kwa niaba ya taifa. Hata kama madhara yalisababishwa na maafisa wa serikali, haitazuiwa kuwafidia waathiriwa.

Taarifa ya Elizabeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version