News
Kenya na Uganda kuimarisha utalii kupitia teknolojia
Serikali ya Kenya na Uganda zimeafikia azimio la ushirikiano ili kuboresha sekta ya utalii kwa kuuza sifa za vivutio vya utalii kupitia mfumo wa teknolojia na uvumbuzi kwa kujumuisha vijana.
Balozi wa Uganda nchini Kenya Paul Mukumbya, alisema nchi hizo mbili zina vivutio tofauti vya utalii ambavyo iwapo zitashirikiana, basi sekta ya utalii itaimarika zaidi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kongamano la nne la maonyesho ya kitalii baina ya Kenya na Uganda mjini Malindi, Balozi Mukumbya alisema ushirikiano huo unalenga kujumuisha vijana katika sekta ya teknolojia ya mtandao ili kutangaza utalii katika mataifa hayo.
Kwa upande wake mwakilishi wa bodi ya kitaifa ya utalii Josephine Mbela alilitaja kongamano hilo kama litakaloboresha uhusiano baina ya mataifa hayo huku akiwahimiza wananchi kuwa huru kutembelea vivutio vya utalii.
Wakati huo huo Gavana wa Kilifi Gedion Mung’aro alisema eneo la pwani lina raslimali za kutosha za kuuza sekta ya utalii kimataifa na kwamba Uganda inasalia nchi ambayo wananchi wake hutembelea Kenya kwa wingi kutalii.
Taarifa ya Joseph Jira