News
Kikao cha wabunge wa UDA na ODM chafanyika Nairobi
Rais William Samoei Ruto pamoja na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wameongoza kikao cha pamoja cha wabunge wa chama ODM na UDA katika eneo la Karen Jijini Nairobi.
Akizungumza katika kikao hicho, Rais Ruto aliwahimiza wabunge wa vyama hivyo viwili kushirikiana ili taifa la Kenya liweze kusonga mbele kimaendeleo na akawataka viongozi kuweka maslahi ya Wakenya mbele kuliko siasa za vyama na ubinafsi.
Rais Ruto alisema ni kupitia umoja ndipo ajenda za serikali zitafanikishwa ipasavyo na kuwapongeza wabunge na Maseneta kwa kupitisha miswada mbalimbali kama wa afya ambao umekuwa wenye manufaa kwa Wakenya.
“Hili sio suala la Williama Ruto. Leo niko kesho sitakuwa. Sio pia kuhusu Raila Odinga bali ni kwa ajili ya nchi inayoitwa Kenya ambapo tuko na fursa nzuri ya kufanya maamuzi yanayofaa kwa ajili ya nchi hii’’ alisema Rais Ruto
Ni kauli ambayo iliungwa mkono na Raila Odinga ambaye aliwataka wabunge wa vyama hivyo kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuafikia hayo.
Taarifa ya Janet Mumbi