Sports

Kikosi cha Wanamichezo wa Para ya Kenya kinazidi kujiandaa kwa Mashindano ya Dunia Yakayofanyika Mjini New Delhi,India

Published

on

Kikosi cha Wanamichezo wa para kutoka Kenya hawachi jambo lolote kwa bahati nasibu wanapojiandaa kwa Mashindano ya Dunia yatakayofanyika mwezi huu mjini New Delhi, India.

Timu hiyo ilifanya mazoezi ya nguvu  katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, ambapo makocha walizingatia kuboresha mbinu na kuongeza kujiamini kabla ya kivumbi cha kimataifa.

Mazoezi hayo yaliwaleta pamoja wanamichezo wa fani mbalimbali ikiwemo mitupo na mbio fupi za uwanjani wote wakiwa na hamu ya kupeperusha bendera ya Kenya kwenye jukwaa la dunia. Kikao hicho kilisisitiza uimara, mbio za kasi, na maandalizi ya kisaikolojia, huku makocha wakiwahimiza wanamichezo kudumisha nidhamu na hali bora ya mwili kadri siku ya mashindano inavyokaribia.

“Tunafanya kazi katika kasi, uimara, na zaidi ya yote nguvu ya kisaikolojia,” alisema Kocha Mkuu Henry Kirwa, akiongeza: “Tunawaomba Wakenya wote wawatie moyo wanamichezo hawa — iwe kazini, mgahawani, au ukiwa nyumbani. Mshikamano wenu unamaanisha kila kitu na utawasukuma kutoa walicho nacho bora kabisa.”

Kwa wanamichezo wengi, mashindano haya ni nafasi ya kurekebisha makosa ya nyuma na kutoa matokeo bora zaidi katika ulingo wa dunia.

“Hadi sasa mazoezi yamekuwa mazuri kama mnavyoona. Mwaka huu hautakuwa kama mingine, mwaka huu utajaa medali,” alisema mtoaji wa tufe, Rajab Chetty.

“Lengo langu ni kuwa wa kwanza na kuleta heshima nyumbani, kama mtoaji wa tufe wa kwanza katika kipengele cha F11. Nataka kuweka historia,” aliongeza.

Mwanariadha wa mbio fupi T47, Stency Neema, naye alisisitiza: “Kambi ni nzuri, tunajiandaa vizuri. Tunaamini tutafanya vyema… safari hii tumejiandaa kikamilifu.”

Maafisa wa timu nao walieleza matumaini kwamba Kenya itatoa matokeo mazuri mjini New Delhi, ikijenga juu ya sifa inayoongezeka ya nchi katika michezo ya para.

“Tumejiandaa kwa dunia, tegemeeni mambo makubwa na tutaliletea taifa fahari. Tegemeeni medali nyingi,” alisema Rais wa KNPC, Ronald Milare.

Timu itaendelea na maandalizi yake maeneo mbalimbali nchini katika siku zijazo, kabla ya kusafiri kwenda New Delhi Septemba 24 kwa ajili ya kuzoea mazingira kabla ya mashindano — yatakayoanza rasmi Septemba 27.

Kwa kuwa wanamichezo bingwa wa para kutoka duniani kote wanatarajiwa kushiriki, tukio hilo litakuwa jaribio kubwa kwa kikosi cha Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version