Business
KTB imeweka mikakati ya kuwavutia wawekezaji wa kimataifa
Serikali ya kitaifa kupitia bodi ya utalii nchini (KTB) imeweka mikakati ya kuwavutia wawekezaji wa kimataifa ili kupanua soko la wageni kutoka mataifa ya nje.
Mwenyekiti wa bodi hiyo Francis Gichaba alisema kutokana na hatua hiyo, idadi ya watalii wanaozuru Pwani itaongezeka hadi zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na nchi zingine zilizonawiri katika sekta ya utalii.
Akizungumza katika kongamano la uekezaji wa utalii eneo la Diani kaunti ya Kwale, Gichaba alisisitiza umuhimu wa waekezaji kuboresha maeneo ya hoteli pamoja na vivutio vingine vya kitalii.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kudhibiti utalii (TRA) Norbert Talam amesema kuwa uboreshaji wa hoteli hizo utainua viwango vya utalii nchini.
Hata hivyo Wadau wa sekta ya utalii wakiongozwa na Hasnain Nooran waliitaka serikali kuu kuongeza safari za ndege za moja kwa moja katika eneo la Pwani.
“Ikiwa Kenya itakuwa na safari za ndege za moja kwa moja kutoka mataifa ya Ulaya hadi Pwani ya Kenya basi itakuwa vizuri zaidi kuimarisha sekta ya utalii nchini kwani tumetegemea pia watalii wa kigeni”, alisema Hasnain.
Taarifa ya Mwanahabari wetu