Sports

Ligi Kuu Epl;Manchester United Bado mambo Hayajatiki,Everton Wakishinda

Published

on

Kilabu ya Manchester United bado hawajapata ushindi wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Fulham Jumapili, huku kilabu ya Everton ikiongozwa na Jack Grealish ikizindua uwanja wao mpya kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Brighton.

Kikosi cha Ruben Amorim kilikosa nafasi muhimu baada ya Bruno Fernandes kupiga penalti nje kipindi cha kwanza, na United wakatoka na alama moja Craven Cottage.

Goli la kujifunga la Rodrigo Muniz liliwapa United uongozi katika dakika ya 60, lakini Emile Smith Rowe aliingia kama mchezaji wa akiba na kuokoa pointi kwa Fulham akifunga dakika ya 73.

Amorim anajaribu kuinua United baada ya kumaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya 15, lakini safu yake mpya ya ushambuliaji yenye thamani ya £200 milioni (takribani Sh bilioni 35), ikiwajumuisha Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko, bado haijazaa matunda.

United walipoteza 1-0 dhidi ya Arsenal kwenye mechi yao ya ufunguzi na sasa watalalamika kupoteza pointi nyingine mbili jijini London.

Fulham, hata hivyo, walihisi wageni walipendelewa na maamuzi mawili tata. Penalti ya United ilitolewa baada ya VAR kuonyesha Calvin Bassey akimvuta Mason Mount, lakini Fernandes alipiga juu ya lango.

Bao lao la kwanza msimu huu lilitokana na kichwa cha Leny Yoro kilichomgonga Muniz na kuingia wavuni, lakini Fulham walikasirishwa VAR kutokuchukua hatua baada ya Bassey kusukumwa.

Smith Rowe alihakikisha Fulham wanapata alama moja baada ya kukamilisha krosi ya Alex Iwobi dakika 17 kabla ya mpira kuisha.


Enzi Mpya ya Everton

Baada ya kuaga kwa hisia uwanja wa Goodison Park, ambao ulikuwa nyumbani kwao tangu mwaka 1892, Everton wanatarajia uwanja wao mpya wenye uwezo wa watazamaji 53,000 kuwarejeshea siku zao za heshima.

Ingawa Everton wameshinda mataji tisa ya ligi kuu — idadi inayopitwa na vilabu vinne pekee — hawajashinda kombe kubwa kwa miaka 30, wakimaliza misimu ya mwisho Goodison wakipambana na kushuka daraja.

“Tunajaribu kusogeza klabu mbele. Hii ni hatua kubwa kwa Everton,” alisema kocha David Moyes.

Grealish, usajili maarufu wa Moyes, alionyesha kipaji kilichomfanya Man City kumlipia Aston Villa £100 milioni mwaka 2021, akipiga pasi za magoli yote mawili.

Iliman Ndiaye, aliyefunga bao la mwisho Goodison mwezi Mei dhidi ya Southampton, aliandika historia nyingine kwa kufunga bao la kwanza kwenye uwanja mpya katika dakika ya 23 baada ya krosi kali ya Grealish.

Brighton walipoteza nafasi nyingi — Kaoru Mitoma akipiga mwamba, Jan Paul van Hecke kugonga nguzo na Danny Welbeck akikosa bao wazi.

James Garner aliongeza la pili mapema kipindi cha pili kwa shuti kali baada ya pasi ya Grealish.

Brighton walipata nafasi ya kufufua matumaini kwa penalti, lakini Jordan Pickford aliokoa mkwaju dhaifu wa Welbeck, na kukamilisha siku ya kumbukumbu kwa Everton.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version