News
LSK yataka mkuu wa kituo cha polisi cha Central-Mombasa kusimamishwa kazi
Chama cha wanasheria nchini (LSK), tawi la Mombasa, kimetaka kusimamishwa kazi mara moja kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Central jijini Mombasa pamoja na maafisa wote waliokuwa kazini wakati wa tukio la kifo cha Simon Warui, kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha akiwa kizuizini kituoni humo.
Kupitia kwa mwenyekiti wake, wakili Natasha Ali Errey, LSK ilitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha na linaloibua maswali mazito kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu.
Wakili Natasha alisema kuna dalili za dhuluma au uzembe wa hali ya juu, hivyo ni muhimu kwa maafisa waliokuwa kazini wakati huo kuondolewa kazini kwa muda ili uchunguzi ufanyike bila vikwazo.
Chama hicho pia kilitaka mamlaka huru ya uangalizi wa polisi (IPOA) kuharakisha uchunguzi kuhusu kifo cha Warui, na kuhakikisha kuwa ripoti yake inatolewa hadharani, kwa uwazi na kwa wakati, ili wananchi waweze kufahamu hatua zitakazochukuliwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, wakili Natasha alisisitiza kuwa LSK haitalegeza kamba katika kufuatilia suala hilo, na itaendelea kushinikiza haki itendeke kwa familia ya marehemu Warui hadi ukweli utakapofichuka.

Simon Warui anayedaiwa kufariki katika kituo cha polisi cha Central, Mombasa.
Awali taarifa ya polisi katika kituo cha Central jijini Mombasa ilisema Warui alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kuanguka kutoka kwa ukuta wa seli alipojaribu kuruka.
Hata hivyo ripoti ya upasuaji wa maiti ilibaini kuwa Warui alifariki kutokana na majeraha na ukosefu wa Oksijeni.
Taarifa ya mwanahabari wetu.