News
Maagizo ya waziri Murkomen yaendelea kuzua mihemko.
Wabunge wanaoegemea chama chake aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua DCP wametangaza mipango ya kuwasilishwa hoja bungeni ya kutaka kutimuliwa madarakani kwa waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen.
Wabunge hao walidai matamshi aliyotoa waziri Murkomen ya kuagiza maafisa wa polisi kupiga risasi na kuua-Shoot to Kill hasa wakati wa maandamano yanatosha kumuondoa ofisini.
Akitangaza mipango hiyo mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji, alimkosoa Murkomen akidai anachochea ongezeko la visa vya mauaji ya kiholela nchini vile vile watu kutoweka katika njia tatanishi.
Mbunge huyo alidai visa hivyo vimekuwa vikishuhudiwa chini ya uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza.
Alishinikiza bunge la kitaifa kutekeleza jukumu lake la uangalizi na kulinda maisha na uhuru wa wakenya.
Murkomen amekuwa akikosolewa kutokana na matamshi yake ya wiki jana baada ya kushuhudiwa uharibifu wa miundombinu ya maafisa wa polisi vile vile baadhi ya maafisa wa usalama kujeruhiwa na waandamanaji, ambapo baadaye alionekana akijitetea.
Taarifa ya Joseph Jira