News
Mahakama kuu yamzuia Kingi na Wetangula kujihusisha na siasa
Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetangula na spika wa bunge la Seneti Amason Kingi wamepigwa breki kujihusisha na mikutano ya kisiasa.
Hii ni kufuatia amri ya Mahakama kuu inayowataka wawili hao kukoma kujihusisha na uhamasishaji wa kisiasa kwa muda wakisubiri kusikilizwa kwa ombi linalopiga shughuli zao lilowasilishwa Mahakamani na Shirika la Vocal Africa.
Jaji wa Mahakama hiyo David Mburu, alitoa amri hiyo akiagiza kuwa ombi hilo lisikilizwe kwa umakini na washtakiwa wote wawasilishiwe stakabadhi za kesi hii leo.
Katika ombi hilo, Shirika la Vocal Africa linadai kuwa ushiriki wa maspika hao katika shughuli za kisiasa unaibua maswali mazito ya kikatiba kuhusiana na uhuru wa bunge na majukumu yaliyowekwa kwa maafisa wa serikali.
Vocal Africa pia limesisitiza kuwa, ingawa kila ana haki ya kuwa na maoni ya kisiasa na kushiriki katika maswala ya kisiasa, maspika wanashikilia ofisi za kikatiba ambazo hazihitaji upendelea bali zinahitaji uhuru wa kitaasisi.
Kwa muda sasa spika Kingi na Wetangula wameonekana katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wakipigia debe ajenda ya rais William Ruto, kinyume na Katiba inayowalazimisha maspika kuangazia masuala ya bunge na shughuli zengine muhimu za kiserikali.
Taarifa ya Elizabeth Mwende