News
Mahakama ya Kilifi yamzuilia mshukiwa wa ulawiti rumande
Mahakama ya Kilifi imeagiza kuzuiliwa rumande kwa mwanaume mmoja aliyekabiliwa na mashtaka ya ulawiti wa mtoto wa umri wa miaka 9.
Akitoa agizo hilo Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike alisema kwamba mshukiwa Hassan Abdulrahman Ali kwa jina maarufu Fadhil anafaa kurudishwa Mahakamani mnamo tarehe 11 mwezi Septemba mwaka huu.
Awali kabla ya agizo hilo, Mahakama ilielezwa kwamba Hassan alitekeleza kitendo hicho cha unyama kwa mtoto huyo mnamo tarehe tofauti kati ya mwezi Aprili hadi tarehe 20 ya mwezi Agosti mwaka huu.
Mahakama pia ilielezwa kwamba mshukiwa alitekeleza unyama huo katika msikiti wa Masjid Rahma uliyoko katika eneo la Mkoroshoni wadi ya Sokoni kaunti ya Kilifi.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 11 mwezi Septemba mwaka huu katika Mahakama hiyo ya Kilifi chini ya Hakimu James Mwaniki.
Taarifa ya Teclar Yeri