News
Mahakama ya mnyima dhamana mshukiwa wa Mihadarati
Mahakama ya Kilifi imeagiza mshtakiwa wa kesi ya usafirishaji wa Mihadarati aina ya bangi kuendelea kuzuiliwa rumande wakati kesi hiyo ikiendelea.
Akitoa agizo hilo Hakimu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa alisema kuwa mshtakiwa anafaa kurudishwa mahakamani mnamo tarehe 19 mwezi Septemba mwaka huu.
Kabla ya agizo hilo kutolewa Mahakama ilielezwa kwamba mnamo tarehe 7 mwezi Agosti mwaka 2024, maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kilifi wakiwa katika ziara ya usalama walikamata gari lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara mjini Kilifi lenye nambari ya usajili KCF 259K aina ya Subaru likiwa limebeba gunia saba za bangi huku dereva wa gari hilo asijulikane aliko.
Kulingani na maelezo ya afisa mchunguzi wa kesi hiyo gari hilo lilipelekwa hadi kituo cha polisi cha Kilifi ambapo mwenye gari ambaye ni Ezra Omondi alijitokeza baadaye na kueleza kwamba alikuwa amelikodisha gari hilo kwa mshtakiwa Reagan Onyango Otieno.

Bangi ya thamani ya mamilioni ya pesa yanaswa mjini Kilifi
Mahakama pia ilielezwa kwamba maafisa wa polisi waliweza kumkamata mshtakiwa mnamo tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka 2024 baada ya mwenye gari kueleza kwamba mshukiwa alikuwa ametorokea katika kijiji cha Dago kaunti ya Kisumu na kisha baadaye kusafirishwa hadi mjini Kilifi katika kituo cha polisi cha Kilifi mnamo tarehe 8 mwezi Oktoba mwaka 2024 na hatimaye kufunguliwa mashtaka.
Mahakama pia ilimnyima dhamana mshukiwa Reagan Onyango Otieno baada ya kusakwa na maafisa wa upelelezi kwa mda mrefu.
Kesi hiyo itaendelea mnamo tarehe 19 mwezi Septemba mwaka huu.
Taarifa ya Teclar Yeri