News
Mahakama ya Mombasa kusikiza kesi ya ulawiti Septemba 8
Mkufunzi wa mchezo wa soka kaunti ya Mombasa Mbarak Swaleh maarufu Coaches amefikishwa katika Mahakamani ya Mombasa akikabiliwa na kosa la ulawiti wa mtoto wa kiume wa umri wa miaka 12 ambaye ni mchezaji katika timu anayoifunza.
Mahakama ilielezwa kwamba Swaleh alitekeleza kitendo hicho kati ya mwezi Januari na Agosti 14, 2025, katika eneo la uwanja wa soka wa Fort Jesus katika eneo bunge la Mvita.
Mahakama pia ilielezwa kwamba mshukiwa alimshawishi mtoto huyo hadi kwenye chumba cha kuhifadhi vifaa vya soka kwa kisingizio cha kuchukua vifaa vya mazoezi kisha akamdhulumu kimapenzi.
Aidha, kocha huyo pia anakabiliwa na shtaka lengine la kutekeleza kitendo kichafu kwa mtoto huyo ambapo tukio hilo lilifichuliwa na mtoto mwenyewe mnamo tarehe 16 Agosti, 2025 baada ya kumueleza mamake mzazi kuhusu unyanyasaji huo.
Akiwa mbele ya Hakimu mkaazi mwandamizi David Odhiambo mshukiwa alikana mashtaka dhidi yake na akaachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki tano pamoja na mdhamini wa kiasi sawa hicho.
Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Septemba 8 mwaka huu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu