News

Mamlaka ya KPA yalalamikia changamoto zinazolemaza shughuli zake.

Published

on

Licha ya Bandari ya Mombasa kuendelea kurekodi matokeo bora katika utendakazi wake,mamlaka ya bandari nchini (KPA) imebainisha kwamba bado kuna changamoto zinazolemaza shughuli zake.

Akizungumza katika kikao na kamati ya bunge kuhusu ushirikiano wa kikanda, mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kuwa changamoto hizo ni pamoja na idadi kubwa ya mashirika yanayokagua mizigo, vizuizi vya kupima uzito wa magari (weighbridges), na vizuizi vya polisi barabarani katika eneo la Kaskazini (Northern Corridor).

Kulingana na nahodha Ruto hali hiyo bado inaathiri ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na biashara kwa ujumla.

Nahodha Ruto pia alieleza athari za ada zisizo rasmi zinazotozwa na mashirika mbalimbali, pamoja na ushuru wa CESS unaotozwa na serikali za kaunti kwa mizigo ambayo tayari imekaguliwa na kulipiwa bandarini.

Aliongeza kuwa gharama hizo za ziada zinaathiri ushindani wa Kenya kama kitovu cha biashara katika ukanda wa afrika mashariki.

Wakati uo huo, Ruto aliitaka serikali kuharakisha uboreshaji wa mifumo ya usafirishaji kwa kuongeza matumizi ya teknolojia na kuunganisha mifumo ya upimaji wa uzito wa magari kote nchini.

Kwa upande wake, kamati ya bunge kupitia kwa mwenyekiti wake, Bi. Irene Mayaka, iliahidi kwamba kamati hiyo itafuatilia kwa karibu malalamshi yaliyoibuliwa na kuhakikisha kwamba suluhu mwafaka inapatikana.

Taarifa ya mwanahabari wetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version