News
Maseneta wahimiza mizozo ya ardhi Pwani kutatuliwa
Kamati ya bunge la seneti kuhusu masuala ya Ardhi, Mazingira na maliasili imeilaumu Wizara ya Ardhi nchini kwa kutowasilisha stakabadhi za ardhi za kaunti ya Kilifi ili kushughulikiwa ndani ya kaunti.
Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo ilisema licha ya kuwepo kwa serikali za ugatuzi, stakabadhi za ardhi za Kilifi bado zimesalia katika kaunti ya Mombasa suala ambalo ni changamoto kwa wakaazi wa Kilifi.
Madzayo alikariri kwamba atashirikiana na viongozi wengine wa kaunti ya Kilifi kuwasilisha mswada bungeni utakaoshinikiza stakabadhi hizo kutumwa katika kaunti ya Kilifi sawa na kushughulikiwa ndani ya Kilifi.
Wakati huo huo aliitaka Serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Ardhi nchini kutatua changamoto ya umiliki wa ardhi za Pwani hasa baada ya rais William Ruto kuahidi kufanikisha mpango huo.
Haya yamejiri wakati wa kikao cha kuzungumzia suala la unyakuzi wa ardhi katika wadi ya Ganda eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu