News

Mashahidi wafichua maovu kwenye kesi ya Shakahola

Published

on

Ushahidi wa kutisha umeendelea kufichuliwa katika kesi ya mauaji ya Shakahola, ambapo Mhubiri tata Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 35 wanakabiliwa na mashtaka mazito ikiwemo ukatili wa watoto, mateso, na unyimwaji wa elimu.

Kesi hiyo iliendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu mkuu Nelly Chepchirchir katika Mahakama ya Watoto ya Tononoka kaunti ya Mombasa huku mashahidi wanne wakitoa ushahidi wao.

Mmoja wa mashahidi, Maxwell Kisienya, ambaye ni Mkurugenzi wa shule ya Bridge International Academy Lungalunga, alieleza kuhusu mwanafunzi aliyetoweka baada ya kuondolewa shuleni kwa kushindwa kulipa karo mnamo tarehe 19 Oktoba 2017 na tokea hapo, shule haikupokea maombi yoyote ya uhamisho, wala hakujulikana alipoelekea mwanafunzi huyo.

Katika ushahidi wa kidijitali, Koplo Joseph Mwai, mtaalamu wa uchunguzi wa kidijitali kutoka Kitengo cha Kupambana na Ugaidi, ameeleza mahakama jinsi alivyovuna taarifa kutoka kwa simu ya shahidi ambapo aligundua picha nne za watu waliokonda kupita kiasi.

Aidha, mtaalamu wa upasuaji wa maiti, Dkt. Richard Njoroge, alithibitisha kwamba miili mingi kati ya ile 453 iliyofukuliwa kutoka makaburi ya halaiki ilikuwa katika hali ya kuharibika kupita kiasi huku akieleza kwamba katika baadhi ya miili, njaa kali ndiyo iliyotajwa kuwa chanzo cha kifo kutokana na ukosefu mkubwa wa uzito wa mwili.

Kwa mujibu wa daktari huyo, sampuli za meno, mifupa na kucha zilichukuliwa kutoka kwa miili hiyo na kufanyiwa vipimo vya DNA, ambapo baadhi ya waathiriwa sasa wametambuliwa kupitia familia zao.

Mahakama pia ilisikiliza ushahidi kutoka kwa Inspekta mkuu Job Wafula Wanyonyi, aliyekuwa miongoni mwa kikosi cha kwanza kilichofika Shakahola kufuatia ripoti za kijasusi, mnamo tarehe 13 mwezi Aprili 2023, ambapo aliwaokoa watu waliokuwa wakiishi kwenye vibanda duni, wengi wao wakiwa dhaifu kiasi cha kushindwa hata kuzungumza.

Aliongeza kuwa baadhi ya watu waliokamatwa walikuwa wakilinda maeneo hayo wakiwa na silaha kama rungu na jembe.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa siku Jumatano, Septemba 17 mwaka huu.

Taarifa ya Mwanahabari wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version