News
Mbunge wa Nyali amepuzilia mbali madai ya kuhusishwa na siasa za ukabila
Mbunge wa Nyali kaunti ya Mombasa Mohamed Ali amepuzilia mbali madai ya kuhusishwa na siasa za ukabila kwenye kaunti hiyo, akisema anafanya siasa zake bila kujali dini, kabila au hata eneo.
Akizungumza huko Nyali, Ali alisema kuna baadhi ya viongozi katika kaunti ya Mombasa, ambao wamekuwa wakiendekeza propaganda za kumhusisha na siasa za migawanyiko ili kumharibia jina taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao wa 2027.
Ali ambaye alitangaza kuwania wadhifa wa ugavana kaunti ya Mombasa, aliwataka viongozi kufanya siasa zao kwa kunadi sera zao kwa wakaazi na maendeleo ambayo watatekeleza na sio kutumia suala la ukabila kuwachafulia wengine jina.
“2017 hakuna mtu aliniita mkabila, 2022 hakuna mtu aliniita mkabila, 2027 wanasema Mohamed Ali ni mkabila.Mimi Mohamed Ali, mimi nauliza nikisimama hapa juu ya gari, niseme kabila zote za Kenya wanaweza pewa nafasi ya ugavana ni kuna makosa?,basi sasa wanazunguka wakisema Mohamed ni mkabila kwasababu ameanza kufungua watu macho’’ alisema Ali.
Aidha, Ali alisema ataendelea kuzuru maeneo mbalimbali ya kauti ya Mombasa kunadi sera zake na kuwataka wakaazi wa kaunti hiyo kuwachagua viongozi wanaofaa ambao wataimarisha kaunti hiyo kimaendeleo.
‘’Mimi nimewaambia nitatembea hii Mombasa kwa uwezo wake mwenyezi mungu kutetea wananchi wa Mombasa’’ aliongeza Ali
Taarifa ya Janet Mumbi