News
MCK:Vituo vingi vya runinga vinapeperusha matangazo kwa lugha ya mama
Baraza kuu la vyombo vya habari nchini MCK limeshinikiza kutengwa kwa shilingi milioni 1.5 ambazo zitatumika kuanzisha mfumo wa ukaguzi wa masuala ya maadili utakaotumia akili mnemba almaarufu AI.
Wakizungumzia suala hilo maafisa wa baraza hilo wakiongozwa na afisa mkuu mtendaji wa MCK David Omwoyo, walisisitiza haja ya kuimarisha uwezo wa baraza hilo, kwa kufuatilia ili kuhakikisha waandishi wa habari ambao walipewa leseni wanazingatia viwango hitajika vya kitaaluma.
Wakiwa mbele ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu mawasiliano, habari na uvumbuzi, walisema kwa sasa Kenya ina vituo 250 vya runinga na vingi vinapeperusha matangazo kwa lugha ya mama.
Omwoyo alisema idadi hiyo inahitaji uwekezaji wa kimkakati wa kupata mfumo bora ambao utaweza kufuatilia, kukagua na kuchuja matangazo kwa haraka, kutoka kwa vyombo hivyo vya habari hasa vile ambavyo vinapeperusha matangazo kwa lugha ya mama.
Baraza hilo lilisema kwa sasa linategemea wachambuzi 37 ambao wanafuatilia kwa njia ya kizamani matokeo ya vyombo vya habari, na kuripoti ukiukwaji wowote wa sheria.
Taarifa ya Janet Mumbi