News
Mkanganyiko waibuka kuhusu kifo cha afisa wa polisi Haiti
Mkuu wa sheria ameiambia mahakama kuwa hana ufahamu kuwa afisa wa polisi Benedict Kabiru alifariki dunia nchini Haiti, kinyume na matamshi ya rais William Ruto katika kikao cha baraza la umoja wa mataifa jijini New York nchini Marekani.
Kabiru, aliyetumwa nchini Haiti chini ya ujumbe wa msaada wa usalama wa kimataifa (MMS) anashukiwa kuuawa na magenge yenye silaha mnamo mwezi machi 2025.
Miezi kadhaa baadaye, huduma ya kitaifa ya polisi nchini ilikuwa bado haijathibitisha kifo chake, ikisema juhudi za kumtafuta zingali zinaendelea.
Familia ilifika mahakamani ikitaka maelezo, ikidai maelezo hayo alizuiliwa na maafisa kutoka ofisi ya mwanasheria mkuu.
Mawakili wanaowakilisha familia hiyo, Jumatano 25, Septemba 2025, waliambia mahakama kwamba kukiri hadharani kwa Rais William Ruto kuwa Kabiru alikuwa miongoni mwa maafisa waliofariki Haiti, kunachukuliwa kuwa ushahidi.
“Ikiwa taarifa ya rais ni sahihi, basi inatupilia mbali ombi la habari kwa kuwa uthibitisho tayari umefanywa katika ngazi ya juu,” mahakama ilisikiza.
Familia ilirejelea taarifa ya Ruto mnamo Septemba 22, 2025 ambapo aliambia Baraza La Umoja Wa Mataifa; “Lazima nitumie hafla hii kuwaenzi maafisa wa Kenya, Samuel Kitwai, Benedict Kabiru na Kennedy Nzuve waliopoteza maisha wakiwa kazini.”
Walalamishi hao waliambia mahakama kwamba jukumu sasa liko kwa mwanasheria mkuu wa serikali kuthibitisha kama msimamo wa rais ni sahihi.
“Ni wakati huo tu ambapo mahakama inaweza kuendelea kushughulikia matokeo ya kuzuia habari,” mahakama iliambiwa

Maafisa wa polisi wa Kenya wakishika doria nchini Haiti
Wakati rais Ruto alitoa taarifa kwa umma katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, Mwanasheria mkuu alisisitiza kuwa haijapokea taarifa kama hizo kutoka kwa utawala wa polisi.
Mkanganyiko huu, walalamishi walipinga na kusema ni madai ambayo yanahitaji ufafanuzi wa haraka.
Hata hivyo mkuu wa sheria aliomba muda zaidi ili kupata taarifa zaidi.
Taarifa ya Joseph Jira