News
Faki: Anzisheni Mahakama ya Kadhi Shanzu
Senata wa kaunti ya Mombasa Mohammed Faki ameitaka idara ya mahakama kuanzisha rasmi huduma za mahakama ya kadhi katika mahakama ya Shanzu kama njia moja ya kupunguza mzigo wa kazi kwenye mahakama ya kadhi ya Mombasa.
Akizungumza jijini Mombasa seneta Faki alisema mahitaji ya huduma hiyo yameongezeka kutokana na ongezeko la kesi kutoka jamii ya waislamu wanaotoka kaunti jirani ikiwepo Kilifi na sehemu nyingine za pwani.
Faki alidokeza kuwa unanzishwaji wa mahakama ya kadhi katika mahakama ya Shanzu kutarahisisha upatikanaji wa haki eneo hilo na kupunguza gharama za usafiri hadi jijini Mombasa.
Vile vile Faki alishinikiza idara ya mahakama kuajiri majaji zaidi na mahakimu wa kutosha katika eneo la pwani, ili kukabiliana na kesi nyingi zinazowasilishwa na wananchi pamoja na kuhakikisha mahakama hizo zinafanyiwa upanuzi.
Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Mombasa Abdhulswamad Sharif Nassir alisema uhaba wa majaji na mahakimu umechangia mirundiko ya kesi mahakamani na kuathiri harakati za kusikiliza na kuamuliwa kwa kesi.
Taarifa ya Joseph Jira