News
Mpango wa kuboresha afya ya macho kuanzishwa kaunti ya Mombasa
Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na shirika la Christian Blind Mission (CBM) imeanzisha rasmi mpango mpya wa kuboresha afya ya macho kwa wakaazi wa kaunti hiyo.
Kupitia mradi unaojulikana kama Vision Impact, shirika hilo linalenga kupunguza matatizo ya uhafifu wa macho kuona, na upofu unaoweza kuzuilika, kwa kuimarisha huduma za afya na kuongeza uhamasishaji katika jamii.
Mradi huo umefadhiliwa na unatekelezwa katika kaunti saba nchini, huku Mombasa ikiwa miongoni mwao, ukilenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu kwa kutambua kuwa ulemavu mara nyingi ni chanzo na pia matokeo ya umasikini.
Mradi huo utajumuisha hamasa kwa jamii na wahudumu wa afya, uchunguzi wa macho shuleni na kwa njia ya kuzuru nyumba hadi nyumba, huku wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo ya kuona wakipewa rufaa kwa matibabu yanayostahili.
Serikali ya Kaunti ya Mombasa iliesema kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya ya macho na bila ubaguzi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu