News
Mshukiwa wa dawa za kulevya akamatwa Mombasa
Maafisa wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya eneo la Pwani wamemkamata mshukiwa mmoja raia wa kigeni anayehusishwa na mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya.
Mshukiwa huyo Okwara Chimezie Emmanuel, raia wa Nigeria, anaaminika kuwa sehemu ya mtandao mpana wa usambazaji wa dawa za kulevya aina ya Heroin katika ukanda wa Pwani.
Kukamatwa kwake kulifuatia taarifa za kijasusi, ambapo maafisa wa usalama kwa ushirikiano na maafisa wa DCI walifanya operesheni maalum katika eneo la Mafisini, Kadzandani kaunti ya Mombasa.
Wakati wa msako huo, maafisa hao walifanikiwa kunasa kiasi kikubwa cha Heroin kilichokuwa kimefichwa kwenye mafungu tofauti, ikiwa na thamani ya takriban shilingi milioni 30.
Polisi wanasema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha dawa hizo pamoja na kuwakamatwa kwa washirika wengine wanaodaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu, wakiwemo raia wa Kenya wanaoshukiwa kusaidia katika usafirishaji wa dawa hizo.
Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani huku maafisa wa Idara ya upelelezi wa jinai DCI wakitarajiwa kuomba muda zaidi wa kukamilisha uchunguzi wao.
Taarifa ya Mwanahabari wetu