News
Mshukiwa wa wizi afariki katika kituo cha polisi Mombasa
Polisi mjini Mombasa wameanzisha uchunguzi kufuatia kifo cha mshukiwa mmoja aliyefariki muda mfupi baada ya kukamatwa na kupelekwa katika kituo kikuu cha polisi cha Central jijini Mombasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, marehemu Simon Warui, mwenye umri wa miaka 35, alikamatwa mjini Mombasa na maafisa kutoka kituo cha polisi cha Urban kufuatia madai ya kumuibia mwajiri wake.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, Warui alionekana dhaifu na mwenye wasiwasi aliwasilishwa kituoni kabla ya kuomba nafasi ili kwenda msalani kujisaidia.
Muda mfupi baada ya kuingia chooni, polisi walisikia kishindo kikubwa na walipofika ndani inadaiwa walimkuta Warui akiwa amelala sakafuni huku damu ikimtoka puani.
Polisi wanadai walimpeleka hospitalini, ambako alithibitishwa kuwa amefariki wakati alipowasili.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Makadara ukisubiri kufanyiwa upasuaji ili kubaini chanzo cha kifo chake.
Aidha polisi walisema kuwa wametoa taarifa kwa mamlaka huru ya kuchunguza utendakazi wa polisi IPOA, kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu