News
Murkomen: Serikali Kuajiri Maafisa wa Polisi elfu 10
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha inaajiri maafisa wa Polisi elfu 10 katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
Akizungumza mjini Kilifi wakati wa ziara yake ya kutathmini maswala ya kiusalama katika ukanda wa Pwani, Waziri Murkomen amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha usalama mashinani.
Murkomen amesema taifa la Kenya limeshuhudia changamoto nyingi za kiusalama kutokana na idadi ndogo ya maafisa wa usalama nchini, akisema juhudi zilizowekwa na serikali zitasaidia kuimarisha usalama kote nchini.
Waziri huyo wa usalama hata hivyo amedokeza kwamba tayari serikali inaendelea na mpango wa kununua magari ya maafisa wa usalama elfu tano ambayo yatasambazwa kwa vitengo mbalimbali vya kiusalama ili kusaidia kuimarisha usalama mashinani.
Kauli yake imejiri baada ya wananchi kulalamika kuhangaishwa na magenge ya kihalifu huku maafisa wa usalama wakishindwa kutekeleza majukumu yao kufuatia idadi ndogo ya maafisa wa usalama sawa na uhaba wa magari ya Polisi.