News
Murkomen: Tutaweka camera za CCTV katika vituo vyote vya polisi
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen ametoa taarifa kuhusu hatua ambazo zimepigwa na wizara hiyo katika kuimarisha usalama.
Akizungumza katika jumba la Harambee jijini Nairobi, Murkomen alisema mageuzi ambayo yamekuwa yakifanywa katika idara ya polisi nchini yamesaidia katika kukabiliana na matukio mbalimbali kama ya kigaidi miongoni mwa mengine.
Murkomen alisema maafisa wa usalama nchini wamekuwa wakiweka juhudi nyingi katika kuhakikisha kuna usalama wa kutosha licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiikumba idara ya usalama nchini katika kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Licha ya kuwa kumekuwa na changamoto nyingi katika kuimarisha usalama nchini, maafisi wa polisi wamekuwa wakijitolea zaidi kuhakikisha kuna usalama na wengine hata kufariki wakiimarisha usalama katika taifa hili’’, alisema Murkomen
Wakati huo huo, Murkomen alisema maafisa mbalimbali ambao wamekuwa wakihusishwa na vifo vya baadhi ya wananchi na hata utekaji nyara, wengi wao walipatikana na hatia na kukabiliwa kisheria
Vilevile, Murkomen alisema wizara ya usalama wa ndani itaweka camera za CCTV katika vituo vyote vya polisi nchini na pia kutakuwa na mfumo wa kidijitali ambao utatumika na wananchi kurekodi taarifa zao kwenye vituo vya polisi.
Taarifa ya Janet Mumbi