News
Murkomen:Kupambana na itikadi kali za kidini kunahitaji juhudi za jamii nzima
Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesisitiza umuhimu wa mbinu ya kuhusisha jamii nzima ili kukabiliana na misimamo mikali ya kidini, akionya kuwa kutegemea polisi pekee hakutatosha kukabiliana na janga hilo ambalo limegharimu maisha ya maelfu ya watu kote nchini.
Murkomen alizungumza kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, akitoa taswira ya uwiano kati ya mauaji ya Shakahola na vifo vya hivi majuzi katika eneo la Kwa Binzaro, akisisitiza umuhimu wa raia kuchukua jukumu kubwa la kulinda jamii zao.
“Mradi tu tunaachana na majukumu yetu kama raia, kutakuwa na masuala ya usalama kila wakati,” Murkomen alisema. “Usalama sio jukumu la polisi pekee. Lazima pia tufanye sehemu yetu. Huwezi kuacha nyumba yako bila kufuli na kutarajia kuwa ni jukumu la polisi pekee.”
Waziri huyo alitaja kushindwa katika miundo ya jamii, kama vile muungano wa kitaifa wa wakaazi (KARA), ambao alisema unapaswa kuchukua jukumu kubwa katika kukusanya na kupeleka taarifa za kijasusi kwa mashirika ya usalama.
Mhubiri tata Paul Mackenzie akiwa katika mahakama ya Shanzu anakokabiliwa na shutuma za mauaji ya msitu wa Shakahola.
Alibainisha kuwa katika kesi ya Shakahola, misimamo mikali ilifikia kiwango kikubwa cha vifo vya njaa, lakini dalili za onyo hazikuonekana.
“Hata baada ya Shakahola, kulikuwa na mtu ambaye alisafiri kutoka Siaya hadi msitu wa Chakama na watoto wake kwa miezi. Je! hakuna mtu aliyegundua?” Murkomen aliuliza, akitoa wito wa umakini zaidi na kuripoti mapema.

Baadhi ya miili iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.
Aidha alifichua kuwa kujidhibiti kwa taasisi za kidini ni sehemu ya hatua za kuzuia kuingizwa kwa itikadi kali.
Afisa mkuu mtendaji wa muungano wa KARA Henry Ochieng, ambaye pia alionekana kwenye mjadala huo, alikiri kuwa ukosefu wa uaminifu kati ya wananchi na polisi inaendelea kutatiza hatua ya umma kutoa taarifa za kijasusi.
“Kuna nia njema kutoka kwa jamii kuunga mkono polisi, lakini pia kuna hofu kwamba taarifa zinazotolewa huenda zikatumiwa dhidi yao,” Ochieng alisema, akiongeza kuwa hali hii ya kutoaminiana sharti ishughulikiwe ili kuboresha ushirikiano.
Taarifa ya Joseph Jira