News
Musyoka, Akosoa Kuvamiwa kwa Gachagua Kasarani
Kinara wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekosoa uvamizi uliofanywa na kundi la vijana wakati wa ibada ya Jumapili katika Kanisa la PCEA Kasarani jijiji Nairobi.
Kalonzo amesema uvamizi huo ulitatiza shughuli za ibada Kanisani na huenda vijana hao walikuwa na malengo ya kumdhuru aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Kalonzo ametaja kitendo hicho kama cha aibu kwa taifa hili ambalo linatambulika na ulimwengu kama taifa lenye kuenzi amani na usalama, uwiano na ushirikiano wa kijamii.
Kiongozi huyo wa Wiper amedai kuchukizwa na jinsi vijana wanavyoweza kusababisha vurugu katika sehemu za ibada, akisema tabia hiyo inafaa kukomeshwa kote nchini.
Katika tukio hilo la siku ya Jumapili, Gachagua amemkashfu Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja akidai kwamba wanahusika moja kwa moja na shambulio hilo hali ambayo ilizua taharuki Kanisani.
Akizungumza baada ya maafisa wake wa kibinafsi na wale wa usalama kuingilia kati swala hilo, Gachagua amedai kushangazwa na baadhi ya maafisa wa polisi kutothubutu kusaidia kuimarisha usalama wakati wa tukio.