Business
Mvua Yaharibu Ubora wa Nyanya Sokoni, Kilifi
Wachuuzi wa nyanya katika soko la Kwa Charo-Maeo, mjini Kilifi, wamelalamikia athari za mvua zinazoendelea kunyesha, wakisema kuwa hali hiyo inasababisha nyanya nyingi kufika sokoni zikiwa zimeharibika, hivyo kuathiri vibaya biashara zao.
Kwa mujibu wa wachuuzi hao, magari mengi yanayosafirisha nyanya kutoka mashambani hufika sokoni yakiwa yamechelewa, kutokana na hali mbaya ya barabara zinazozuia magari kuingia mashambani kwa urahisi, hasa wakati wa mvua kubwa ambapo matope huziba njia.
Licha ya kuwa nyanya zinapatikana kwa wingi msimu huu, wachuuzi hao wanasema wanalazimika kuuza kwa bei ya juu ili kufidia hasara wanayopata kutokana na upotevu wa bidhaa zilizoathirika na ucheleweshaji wa usafirishaji.
Wakati huo huo, wametoa wito kwa serikali kuu na ya kaunti kuchukua hatua za haraka kurekebisha barabara mbovu zinazoelekea mashambani ili kuwezesha usafirishaji wa bidhaa kwa wakati. Wamesisitiza kuwa hali ya sasa inawaumiza kibiashara, na pia inaweza kuchangia kupanda kwa gharama ya vyakula kwa walaji.