News
Machifu waliotekwa na alshabab Mandera kutuzwa na rais Ruto
Waziri wa usalama wa kitaifa Kipchumba Murkomen amesema machifu watano wa kaunti ya Mandera waliotekwa nyara na wanamgambo wa alshabab mnamo mwezi Februari, 2025 na kuachiliwa huru watatuzwa na rais William Ruto kwa ustahamilivu na kujitolea.
Murkomen alitoa tangazo hilo akipuuza madai ya upinzani kuwa serikali inakula njama na makundi ya ugaidi.
Akizungumza katika kongamano la jukwaa la usalama mashinani eneo la Elwak, Murkomen alisema wapinzani wanachukulia kwa mzaha masuala mazito ya usalama.
Machifu hao walitekwa wakati walipokuwa wanasafiri kutoka Wargadud kuelekea Elwak- Mandera Kusini, kwa shughuli za maandalizi ya ziara ya rais William Ruto eneo la Kaskazini Mashariki.
Gari walimokuwa wakisafiria liliendeshwa kuelekea nchini Somalia kabla ya kuachiliwa baadaye na watu ambao kufikia sasa hawajafahamika.
“Wengine hata walikuwa wananitusi ati wakati machifu walitoka hapa wakachukuliwa na alshabab mpaka upande ule ati sasa sisi kwa sababu machifu kurejeshwa ni sababu mimi na rais tunafanya kazi na alshabab, hawa machifu wote watapata tuzo ya rais, watatambuliwa na serikali kwa sababu ya ujasiri wao wa kupitia shida nab ado wamerudi kufanya kazi”, alisema Murkomen.
Taarifa ya Joseph Jira