News

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani afariki baada ya kuzama maji Vidazini-Kilifi

Published

on

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani mjini Kilifi ameaga dunia wakati akiogelea katika ufuo wa bahari hindi wa Vidazini katika eneo bunge la Kilifi Kazkazini kaunti ya Kilifi.

Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, walisema Mwanafunzi huyo wa mwaka wanne aliyekuwa anasubiri kuhitimu amefariki katika ufuo huo baada ya kuzidiwa na mawimbi makali licha ya waokozi kupiga mbizi ili kumuokoa.

Akizungumza na Wanahabari, Rais wa Wanafunzi wa chuo hicho cha Pwani Athony Muteti amewatahadharisha wanafunzi wenzake kuwa makini wakati wanapofika katika ufuo wa bahari hindi kujivinjari huku akiwarai kuwashauri maafisa wa uokozi pindi wanazuru katika fuo hizo.

Muteti aliwahimiza wanafunzi pamoja na wananchi kuhakikisha wanatii wanachoambiwa na waokozi wa baharini pindi wanapofika katika fuo hizo za bahari kujivinjari, ili kuzuia kushuhudiwa kwa maafa.

Maafisa wa usalama pamoja na wale wa Idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI walifika katika eneo la tukio na kuthibitisha kwamba mwanafunzi huyo alikuwa ameaga dunia, na kuwarai wananchi kuwa waangalifu pindi wanapozuru fuo za bahari hindi kujivinjari.

Mwili huo marehemu ulichukuliwa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika makafani ya hospitali kuu ya rufaa ya mjini Kilifi katika kaunti ya Kilifi.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version