Sports
Mwanariadha Ruth Chepngetich apigwa marufuku miaka mitatu kwa kosa la kutumia dawa zilizopigwa marufuku
Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon kwa wanawake, Ruth Chepngetich, amepigwa marufuku kwa muda wa miaka mitatu baada ya kukiri makosa ya kukiuka sheria za kupinga matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Chepngetich alisimamishwa kwa muda mnamo Julai baada ya sampuli yake kuonyesha matokeo chanya ya dawa ya Hydrochlorothiazide (HCTZ) dawa iliyopigwa marufuku inayotumika mara nyingi kuficha matumizi ya dawa nyingine za kuongeza nguvu katika kipimo kilichochukuliwa Machi 14.
Hata hivyo, mafanikio ya Chepngetich yaliyopatikana kabla ya tarehe hiyo, ikiwemo rekodi yake ya dunia ya muda wa saa 2:09:56 iliyowekwa mjini Chicago mnamo Oktoba 2024, yataendelea kutambuliwa.
Kitengo cha Uadilifu cha Riadha (AIU) kilikuwa kimetaka adhibiwe kwa miaka minne, lakini adhabu yake ilipunguzwa hadi miaka mitatu baada ya kukiri kosa hilo.
Hata hivyo, AIU itaendelea kuchunguza ushahidi uliopatikana kwenye simu ya Chepngetich, ambao unaonyesha “tuuma zenye msingi kwamba matokeo chanya yanaweza kuwa ya makusudi” — ikiwemo ujumbe wa maandishi unaorudi nyuma hadi mwaka 2022.
Mkurugenzi wa AIU, Brett Clothier, alisema:
“Kesi kuhusu kipimo chanya cha HCTZ imekamilika, lakini AIU itaendelea kuchunguza ushahidi wa kutiliwa shaka uliopatikana kwenye simu ya Chepngetich ili kubaini kama kulikuwa na ukiukaji mwingine wowote.”
‘Hakuna aliye juu ya sheria’
Wakati akihojiwa na AIU mwezi Aprili, Chepngetich mwanamke wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa 2:10 alishindwa kutoa maelezo kuhusu matokeo chanya ya kipimo hicho.
Ingawa kiwango cha chini cha kuripotiwa cha HCTZ ni nanogramu 20 kwa mililita moja ya mkojo (20 ng/mL), sampuli ya Chepngetich ilionyesha kiwango cha takriban 3,800 ng/mL.
Pia, chembechembe za HCTZ chini ya kiwango cha kuripotiwa zilibainika katika sampuli nyingine iliyochukuliwa Februari 28, wiki mbili kabla ya kipimo chanya.
Katika mahojiano ya Julai 11, Chepngetich aliwasilishwa na ushahidi wa kutiliwa shaka uliopatikana kwenye simu yake. Wakati huo, AIU ilikuwa imebaini kwamba uwezekano wa “uchafuzi” wa sampuli haukuwa kweli.
Mnamo Julai 31, Chepngetich alibadilisha maelezo yake, akidai kuwa alimeza dawa ya mfanyakazi wake wa nyumbani — ambayo ilibainika kuwa na HCTZ baada ya kuugua siku mbili kabla ya kipimo chake chanya.
AIU ilisema ilikuwa na “mashaka makubwa kuhusu ukweli wa maelezo mapya hayo,” ikiongeza kuwa kwa mujibu wa sheria za kupinga dawa za kuongeza nguvu, “uzembe kama huo” unachukuliwa kama “nia isiyo ya moja kwa moja,” inayostahili adhabu ya miaka minne.
Hata hivyo, adhibu hiyo ilipunguzwa kwa mwaka mmoja baada ya Chepngetich kukiri kosa ndani ya siku 20 zinazohitajika.
Marufuku yake ya miaka mitatu ilianza Aprili 19, siku ambayo alikubali kusimamishwa kwa hiari, na matokeo, tuzo, vyeo, zawadi, na fedha za ushindi kutoka Machi 14 kufutwa.
Mwenyekiti wa AIU, David Howman, alisema kesi hiyo imedhihirisha kwamba:
“Hakuna aliye juu ya sheria.”
Aliongeza:
“Ingawa ni jambo la kusikitisha kwa wale waliomwamini, mfumo huu umeundwa kufanya kazi kwa njia hii. Tasnia ya mbio za barabarani inapaswa kupongezwa kwa kufadhili kwa pamoja juhudi za kupambana na dawa za kuongeza nguvu ambazo zinaweza kubaini makosa hata kwa wanariadha wa kiwango cha juu.”