Sports
Ndoto ya Harambee Stars ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 Yagonga mwamba baada ya kupigwa 3-1 na Gambia Kasarani
Ndoto ya Harambee Stars ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA 2026 ilizimwa rasmi hapo jana baada ya kuchapwa mabao 3-1 na The Scorpions ya Gambia katika mechi ya kufuzu ya Kundi F la CAF iliyochezewa Uwanja wa Kasarani.
Scorpions, wakiongozwa na kocha wa zamani wa Gor Mahia Jonathan McKinstry, walitoa mchezo wa kiukatili katika kipindi cha kwanza dhidi ya vijana wa Benni McCarthy, na kuhuisha matumaini yao ya kufuzu kwa fainali zitakazofanyika Marekani, Kanada na Mexico.
Harambee Stars, waliokuwa na matumaini finyu ya kufuzu, walizidiwa maarifa na upande wa Gambia uliokuwa makini zaidi, uliodhibiti mchezo ndani ya dakika 30 za kwanza.
Udhaifu wa safu ya ulinzi ya Kenya ulionekana mapema dakika ya 12 pale Sulayman Sinyan alipofunga kwa kichwa akimalizia kona ya ndani ya Yankuba Minteh, mshambuliaji wa Brighton & Hove Albion, na kuwaweka Stars kwenye presha.
Minteh, aliyewasumbua mabeki wa Kenya mara kwa mara, aliongeza bao la pili dakika ya 26 kwa shuti la utulivu lililokwenda chini kushoto baada ya kuchukua faida ya makosa ya safu ya kiungo ya Kenya.
Gambia waliongeza bao la tatu dakika ya 38 kupitia Musa Barrow aliyepiga shuti kali la volley lililoenda moja kwa moja hadi kona ya mbali ya goli, na kufunga rasmi mchezo.
Safu ya ulinzi ya Kenya iliendelea kuonekana dhaifu, na hasira zikadhihirika katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza pale Collins Sichenje alipokumbwa na kadi ya njano kufuatia rafu mbaya – hali iliyomwacha kocha McCarthy akiwa mwenye hasira pembeni mwa uwanja.
Stars walionekana kufufuka baada ya mapumziko kufuatia mabadiliko mawili ya wachezaji yaliyoongeza nguvu, na juhudi zao ziliwalipa dakika ya 81.
Ryan Ogam, aliyeingia kutoka benchi, alipiga shuti kwa mguu wake dhaifu wa kulia katikati ya kisanduku na kufunga bao lililoleta matumaini kwa wenyeji.
Hata hivyo, ilikuwa ni kuchelewa mno kwani wageni waliweza kudhibiti mchezo hadi mwisho na kuondoka na alama zote tatu.
Matokeo hayo yanaiweka Kenya ikiwa na pointi 6 pekee katika Kundi F, na ndoto yao ya Kombe la Dunia 2026 ikizimika rasmi licha ya kubakisha mechi tatu.
Kwa upande wa Gambia, ushindi huu uliwapandisha juu ya Kenya na kuweka hai matumaini yao ya kufuzu, ingawa wanakabiliwa na changamoto kubwa dhidi ya Burundi na Gabon.
Kwa Kenya, macho sasa yanaelekezwa kwenye mchezo wa nyumbani dhidi ya UShelisheli siku ya Jumanne ambapo watatumai kumaliza mapumziko ya kimataifa kwa ushindi, huku wakiangazia maandalizi ya kampeni ya AFCON 2027.