News
ODM yatishia kujiondoa katika serikali jumuishi
Huenda mpango wa serikali jumuishi uliobuniwa na rais William Ruto na aliyekuwa Kinara wa chama cha ODM hayati Raila Odinga ukavunjika iwapo masuala ibuka yaliyowasilishwa na Chama cha ODM yatakosa kutimizwa.
Chama hicho kimekosoa jinsi baadhi ya wafuasi wa chama cha UDA kujitenga na mwenzao wa ODM licha ya kuwepo na mpango wa serikali jumuishi pamoja na kukosoa kutishiwa kwa baadhi ya viongozi wa ODM kujiondoa na chama hicho ili wajiunge na UDA.
Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kitaifa Junet Mohammed alisema kuna njama ya kusambaratishwa kwa ushawishi wa chama cha ODM katika maeneo ya Nyanza na Pwani kwani kuna taarifa kwamba baadhi vya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakishurutishwa na maafisa wa Ikulu ya rais.
Junet ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki, alisisitiza kwamba ODM kujiunga na UDA haikuwa na makusudi bali serikali ilihitaji msaada wa viongozi wa chama hicho ili kulinusuru taifa kwani lilikuwa linaelekea mahali pabaya.
“Hatuko kwa serikali jumuishi kimakosa ama kimakusudi wala kwa mualiko bali tuliingia katika serikali jumuishi kutokana na serikali ya rais Ruto kutaka msaada watu ili kulinusuru taifa lakini kama uongozi wa UDA unaona kumetengeza misingi na umaarufu mashinani tunaweza kuwaacha watengeze serikali yao mwaka 2027”, alisema Junet.
Kiongozi huyo ambaye pia ni Mwanachama wa Kamati kuu ya chama hicho alisema wataisha mkutano wa dharura wa Kamati kuu ili kuangazia suala hilo kwani mvutano huo huenda ukazidi kushamiri iwapo hakutakuwa na mikakati mwafaka.
Katika siku za hivi majuzi katika siasa za mashinani, chama cha UDA kimeonekana kikiendeleza siasa za kuimarisha chama hicho pamoja na kusajili wanachama wapya ili kujienga umaarufu zaidi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Viongozi wa UDA walionekana kutangaza hadharani kwamba hakutakuwa na mpango wa kusimamisha mgombea mmoja katika eneo kwenye serikali jumuishi yaani Zoning bali kila kiongozi akijipange kisiasa na kupambana katika nyadhfa anayoelenga kushikilia wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi