News
Ofisi ya ODPP imehitimisha rasmi kesi ya Mackenzie
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imehitimisha rasmi kesi yake dhidi ya mauaji ya Shakahola, ambapo Mhubiri tata Paul Mackenzie na wenzake 35 wanakabiliwa na mashtaka ya unyanyasaji, mateso na ukiukaji wa haki za watoto.
Kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama ya watoto ya Tononika jijini Mombasa mbele ya Hakimu mkuu Nelly Chepchirchir ilianza mnamo tarehe 24 Julai 2024, na kukamilika ramsi kwa uwasilishaji wa mashahidi kutoka upande wa mashtaka.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Mkurugenzi msaidizi wa mashtaka ya umma, Jami Yamina, Victor Owiti, Betty Rubia, Biasha Khalifa, na Eunice Odongo katika kipindi cha kesi, waliwasilisha mashahidi 75 ambao walieleza vitendo vya unyanyasaji, mateso, na kukataliwa kwa haki ya elimu, ambayo yalifanyika katika Shakahola.
Mashahidi watatu akiwemo mtaalamu wa uchambuzi wa data kutoka kampuni ya mawasiliano ya Safaricom Dennis Muriithi walitoa ushahidi wao Mahakamani.
Muriithi amethibitisha kwamba baada ya kupata agizo kutoka kwa Mahakama walifanikiwa kufuatilia namba za simu zinazomilikiwa na Mackenzie, na kutoa taarifa za muhimu kwa uchunguzi.
Shahidi mwengine Israel Veronica, mwenye umri wa miaka 21 kutoka Chakama, mjini Malindi, ameelezea jinsi alivyolazimishwa na baba yake kuacha shule mwaka 2019, na baadaye familia yao ikahama kutoka Nairobi hadi Shakahola baada ya kuuza mali zao.
Naye Inspekta Phoebe Okomo kutoka Kitengo cha Ulinzi wa Watoto cha DCI Mombasa amesimulia kuhusu uokoaji wa watoto 27 kutoka Malindi, akielezea mazingira magumu waliyokuwa nayo watoto hao wakiwa Shakahola, ikiwemo kukosa chakula, kuteswa, na kupigwa.
Kesi hiyo itajadiliwa tena tarehe 14 Oktoba 2025 kwa ajili ya kuthibitisha kama maandiko ya kesi yameandikwa kwa ajili ya kuwasilishwa Mahakamani.
Taarifa ya Mwanahabari wetu