News
Pengo katika uhamasishaji wa afya ya uzazi kilifi
Idadi kubwa ya wanawake na wasichana katika kaunti ya Kilifi bado hawajahamasishwa vilivyo kuhusu masuala ya afya ya uzazi na haki yao ya kupata huduma bora ya afya hasa katika maeneo ya mashinani.
Katika kikao ambacho kiliongozwa na shirika la Timiza Youth Initiative kwenye ukumbi wa Kibaoni mjini Kilifi kaunti ya Kilifi na kuhudhuriwa na vijana, wahudumu wa afya na wadau mbalimbali, ilibainika kuwa afya ya wanawake haijakumbatiwa vilivyo katika jamii hali ambayo imekuwa ikifanya wengi wao kupitia changamoto nyingi na hata kufariki dunia wakati wa ujauzito na wanapojifungua.
Akizungumzia hilo Brian Mundia ambaye ni mwenyekiti wa shirika hilo alisema wasichana wenye umri mdogo pia hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu athari ya kupanga uzazi na kuavya mimba.
Mundia pia alisema vijana wengi wanaogopa kufika katika vituo vya afya kupata ushauri kutokana na hali ya unyanyapaa .
Kwa upande wake Doris Waithira Mzee wa kijiji eneo la Mnarani na ambaye pia anatoa ushauri nasaha kwa wanarika alisema akina mama wengi hawaendi hospitalini kujifungua hali ambayo pia huwa inahatarisha afya ya mtoto.
Kwa pamoja walieleza changamoto zilizopo katika kuwafikia wanawake walioko mashinani ili kutoa hamasa na kutoa wito kwa mashirika na serikali kupitia idara ya afya kushirikiana ili kuhakikisha masuala ya afya ya uzazi na afya ya mama katika jamii inakumbatiwa vilivyo.
Taarifa ya Janet Mumbi