News
Rais Ruto afanya mabadiliko jeshini
Rais William Samoei Ruto amempandisha cheo Meja Jenerali David Kipkemboi Ketter hadi cheo cha Luteni Jenerali na kumteuwa kuwa Kamanda mpya wa Jeshi la nchi Kavu.
Katika taarifa ambayo ilichapishwa siku ya Ijumaa tarehe 27 Juni 2025, katika gazeti rasmi la serikali, Ketter anachukua nafasi ya Luteni Jenerali David Kimaiyo Chemwaina Tarus, ambaye amepelekwa katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Ulinzi nchini (NDU -K) kama Naibu Chansela wa chuo.
Rais Ruto pia alimteuwa Meja Jenerali Benard Waliaula kuwa Kamanda wa Jeshi la wanahewa la Kenya na anachukua nafasi ya Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed ambaye muda wake wa kuhudumu umefikia kikomo baada ya miaka 42 ya utumishi wake.

Meja Jenerali Benard Waliaula
Hadi kuteuliwa kwake kama Kamanda wa Jeshi la wanahewa la Kenya, Meja Jenerali Benard Waliaula alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya ulinzi.
Rais Ruto pia alimpandisha cheo na kumteuwa Brigedia Joel Muriungi M’arimi hadi cheo cha Meja Jenerali na kumteua kuwa Mkuu wa Chuo cha Kijeshi cha Kenya.
Vile vile Rais Ruto alimpandisha cheo na kumteuwa Brigedia Joyce Chelang’at Sitienei hadi cheo cha Meja Jenerali.
Taarifa ya Janet Mumbi