News
Rais Ruto amebuni jopo la kukabiliana na ufisadi
Rais William Ruto amebuni jopokazi la pamoja linaloshirikisha idara mbalimbali nchini na mashirika ya kiserikali ili kupiga jeki vita dhidi ya ufisadi nchini.
Jopokazi hilo linahusisha asasi za kiusalama ikiwemo idara ya ujasusi nchini NIS, idara ya upepelezi wa jinai nchini DCI, Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, na Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP.
Taasisi zengine ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria mkuu, Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA, Benki kuu ya Kenya, Mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za umma, Kituo cha kutoa taarifa za fedha na mamlaka ya urejeshaji wa mali ya umma.
Rais Ruto ambaye aliondoka humu nchini na kuelekea taifa la Japan kwa ziara ya siku tatu, amesema vita dhidi ya uvujaji wa mali ya umma ni lazima ukomeshwe kwani umeathiri pakubwa uchumi wa taifa.
Hatua hiyo ya rais imejiri siku moja baada ya kuwashambulia wabunge na maseneta, akidai kwamba baadhi yao wamekuwa wakishiriki ufisadi ili kuwasuru magavana pamoja na kupitisha miswada bungeni.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi