News

Rais Ruto atangaza siku 7 za taifa kuomboleza kifo cha Odinga

Published

on

Rais William Ruto ametangaza siku 7 za taifa kuomboleza kifo cha Raila Amollo Odinga pamoja na bendera ya taifa kupeperushwa nusu mlingoti katika ofisi zote za umma na balozi za Kenya kwenye mataifa ya ugahibuni.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Ruto amesema mazishi ya Marehemu Odinga yatakuwa ya kitaifa na jukumu hilo litatekelezwa na Wanajeshi chini ya uongozi wa Mkuu wa majeshi nchini Charles Kahariri.

Kiongozi wa nchi, ametaja kamati ya mipango ya mazishi ya Odinga ambayo itaongozwa na Naibu Rais Prof Kithure Kindiki kwa ushirikiano na Kakake mkubwa Odinga, Seneta Oburu Oginga pamoja na familia ya Odinga na viongozi wengine.

“Kutokana na kifo cha Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, kutakuwa na siku 7 za kuomboleza kifo cha ndugu yetu na Kamati ya mipango ya mazishi itaongozwa na Naibu Rais Prof Kithure Kindiki na Kakake Odinga, Seneta Oburu Oginga na atapewa heshima ya kitaifa ikiongozwa na wanajeshi”, alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa nchi, hata hivyo amesema mkuu wa mawaziri nchini Musalia Mudavadi, Waziri wa madini Hassan Ali Joho, Kiongozi wa wengi bungeni Kimani, Ichungwah, na kiongozi wa wachache bungeni Junet Mohamed, Mke wa Odinga Mama Ida Odinga na baadhi ya familia ya Odinga wataondoka nchini hadi India kwa mipango ya usafirishaji wa mwili wa Odinga hadi Kenya.

Wakati huo huo ametoa risala za rambirambi kwa familia ya Odinga na wakenya kwa jumla na kutaja kama kiongozi aliyekuwa mkakamavu na kupigania demokrasia huku akiwataka wakenya kuwa na utulivu wakati mipango ya mazishi inapoendelea.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version