News
Rais Ruto azindua malipo ya bilioni 4.4 kugharamia matibabu ya wakenya kupitia SHA
Rais William Samoei Ruto amezindua malipo ya shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya gharama ya matibabu ya wakenya milioni 2.2 wasiojiweza chini ya mpango wa bima ya afya ya SHA.
Akizungumza katika ikulu ya Nairobi, wakati wa uzinduzi huo Rais Ruto alisema mpango huo unalenga kutoa huduma za afya bila malipo kwa wakenya wasiojiweza kifedha.
Rais Ruto alisema ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya afya kwa wote na ya mageuzi mapya ya sekta ya afya nchini.
Aidha, Rais Ruto alisema hakuna Mkenya ambaye atahangaika kutokana na ukosefu wa huduma za matibabu kutokana na hali ya umasikini.

Wahudumu wa afya ya nyanjani na wakenya wahuhudhuria uzinduzi wa malipo ya shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya gharama ya matibabu ya wakenya milioni 2.2 wasiojiweza chini ya mpango wa bima ya afya ya SHA.
“Tuko na mahospitali elfu tisa, unaweza sasa kuenda kwa hospitali yoyote miongoni mwa hizo ili upate huduma za matibabu’’ alisema Rais Ruto.
Wakati huohuo, Rais Ruto alisema kufikia sasa ni takribani Wakenya milioni 26 ambao wamesajiliwa kwenye bima hiyo na zaidi ya milioni 5.5 tayari wanapokea huduma za matibabu kote nchini na fedha hizo zitatumika kugharamia huduma za matibabu kwenye hospitali za umma na zile zilizoorodheshwa.
‘’Hiyo pia itatusaidia kuondoa mambo ya ukora kule ndani na ufisadi’’ aliongeza Rais Ruto.
Naye waziri wa afya nchini Aden Duale alisema hospitali ambazo zitapatikana na visa vya ulaghai zitakabiliwa kisheria.
Taarifa ya Janet Shume