News

Serikali yatangaza mpango wa kuongeza mgao wa mafuta kwa magari ya polisi

Published

on

Serikali imetangaza mpango wa kuongeza mgao wa mafuta ya Petroli na diseli ya kila mwezi kwa magari ya polisi kutoka lita 450 za sasa hadi lita 650, ili kupunguza changamoto za kiutendaji zinazowakabili maafisa wa usalama kote nchini.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alitoa ahadi hiyo wakati wa mkutano wa Jukwaa la Usalama uliofanyika katika Kaunti ya Homa Bay, baada ya maafisa kulalamikia uhaba wa mara kwa mara wa mafuta unaosababisha magari ya polisi kusimama kabla ya mwezi kuisha.

Kwa mujibu wa Murkomen, marekebisho hayo yatafanywa chini ya mpango unaoendelea wa ukodishaji wa magari ya polisi.
Murkomen alikiri changamoto hizo zipo na kubainisha kuwa uhaba wa mafuta umesababisha wananchi kuwa na dhana potovu kuhusu mienendo ya polisi.

“Maafisa wetu wa polisi wanapowaambia wananchi kwamba ‘gari haina mafuta, hatuwezi kuja,’ watu hufikiria afisa anaomba hongo, lakini si kweli,” alisema Murkomen.

Waziri huyo alifafanua kuwa hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya mashinani ambapo maafisa hulazimika kusafiri umbali mrefu ili kwenda kuchukua mafuta.

“Kwa mfano, askari wa polisi wa Kibish anaposafiri hadi Kitale kuchukua mafuta, akirudi mgao huo haudumu hata siku kumi. Baada ya hapo gari hubaki limeegeshwa hadi mwezi uishe,” aliongeza Murkomen.

Ili kutatua tatizo hilo, Murkomen alisema serikali haitaimarisha mgao huo pekee hadi lita 650, bali pia itasambaza vituo vya mafuta kwa ukaribu zaidi.

Alitaja Marsabit na Moyale kama miongoni mwa maeneo ambayo hivi karibuni yatakuwa yakipata mafuta kwa karibu badala ya kusafiri hadi miji ya mbali kama Nanyuki.

Taarifa ya Elizabeth Mwende

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version