Sports
Torres aibeba Barcelona kwa mabao mawili, Atletico yakwama kwa sare na Mallorca
Mshambulizi Ferran Torres alifunga mabao mawili kwa mabingwa Barcelona walipoichapa Getafe 3-0 Jumapili na kusalia nyuma ya Real Madrid kileleni mwa La Liga.
Dani Olmo pia alifunga bao kwa upande wa Wacatalunya, ambao sasa wako pointi mbili nyuma ya vinara Madrid baada ya kikosi cha Xabi Alonso kuishinda Espanyol Jumamosi na kudumisha rekodi yao ya ushindi wa asilimia 100.
Mwanzo wa msimu wenye kusuasua kwa Atletico Madrid uliendelea baada ya kutoka sare ya 1-1 na Mallorca, huku mshambuliaji wao Julian Alvarez akikosa penalti.
Wakicheza tena katika uwanja wa Johan Cruyff wenye uwezo wa watazamaji 6,000 ulio karibu na kituo chao cha mazoezi, wakati klabu ikisubiri leseni za kufunguliwa kwa uwanja wao uliokarabatiwa wa Camp Nou, Barcelona walitawala mchezo dhidi ya Getafe waliokuwa wakicheza bila ubunifu.
Licha ya kufunga mabao mawili dhidi ya Newcastle kwenye Ligi ya Mabingwa, kocha Mjerumani Hansi Flick alimwacha Marcus Rashford benchi, huku vyombo vya habari vya Uhispania vikiripoti kwamba ilikuwa kwa sababu mshambuliaji huyo wa England alichelewa kwenye kikao cha asubuhi.
Flick tayari amewahi kuwaadhibu wachezaji wengine kwa kosa kama hilo hapo awali, akiwemo beki Jules Kounde.
“(Mzunguko wa wachezaji) ni jambo la kawaida kwa sababu kila baada ya siku tatu au nne tunakuwa na mechi, tunahitaji miguu mipya uwanjani,” Flick alisema alipoulizwa kwa nini Rashford hakuanza.
Mbadala wa Rashford, aliyemrithi kijana nyota aliyeumia Lamine Yamal, alikuwa Torres — na alitumia nafasi yake ipasavyo.
“Tunazo mechi nyingi kwa hiyo ni jambo jema kuwa na kila mchezaji akicheza kwa kiwango hiki,” Flick aliongeza.
Mchezaji huyo wa Uhispania alifungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali baada ya mpira uliopigiwa kisigino na Olmo ndani ya boksi.
Bao la pili la Torres lilikuwa zuri zaidi, akielekeza mpira kwa ustadi pembe ya kushoto chini ya lango baada ya kupigiwa pasi safi na Raphinha.
Mbele, alikaribia kutia kapuni hat-trick ya kipindi cha kwanza alipogonga mwamba kwa shuti kali.
Wachezaji kadhaa wa Barca walionekana kukasirika kabla ya mapumziko baada ya Getafe kufanya makosa mengi ya rafu kali, huku Kounde akiwa mhanga zaidi.
Flick alimpumzisha Raphinha na kumwingiza Rashford kipindi cha pili, huenda kumlinda Mbrazil huyo asipate kadi nyekundu.
“Mara nyingi hawajaribu chochote isipokuwa makosa ya rafu nyingi, kwa maoni yangu, lakini tuliweza kushughulikia vizuri,” Torres aliambia DAZN.
“Niliwaambia wachezaji: lazima tuzingatie mchezo wetu, si wao,” alisema Flick.
Rashford alisaidia bao la tatu la Barcelona, akipenya upande wa kulia na kumpasia Olmo pasi safi ya kufunga, kisha yeye mwenyewe akijaribu mara mbili lakini akazuiwa na kipa wa Getafe, David Soria.
Habari mbaya pekee kwa Barca ilikuwa mchezaji wa akiba Fermin Lopez kuonekana kupata jeraha dakika za majeruhi.
Atletico Wakata Tamaa
Mapema, Atletico walikwama kwa sare dhidi ya Mallorca licha ya kuwazidi wenyeji.
Kikosi cha Diego Simeone kilipunguzwa hadi wachezaji 10 baada ya Alexander Sorloth kuonyeshwa kadi nyekundu, lakini walitangulia kwa bao la Conor Gallagher kabla ya Vedat Muriqi kusawazisha dakika ya 85.
Kilabu hiyo ikisalia nafasi ya 14 mpaka sasa ligi ya LALIGA na alama 5