News
Utata wa uongozi wakumba kanisa la Wesley, Mombasa
Waumini wa kanisa la Wesley Methodist kaunti ya Mombasa wametoa wito kwa usimamizi wa kanisa hilo kutafuta suluhu la kudumu kutokana na mvutano ambao umekuwa ukishuhudiwa mara kwa mara kuhusu uongozi.
Siku ya Jumapili 27, Julai 2025 kulishuhudiwa mvutano kwenye makao makuu ya kanisa hilo baada ya baadhi ya waumini kuzuiliwa kuingia katika kanisa hilo kushiriki ibada ya jumapili.
Kulingana na baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo, waumini hao walizuiliwa kuingia katika kanisa hilo baada ya kupinga uteuzi wa askofu mpya Stephen Kanyaru.
Kwenye kikao na waandishi wa habari askofu David Ochami alikashifu kitendo hicho na kusema ni lazima kuwe na usawa kwa kila mmoja katika nyumba za ibada.
“Tunaenda mahali ya kwamba nyumba ya Mungu itakuwa ni ya watu flani jambo ambalo ni kinyume cha neno la Mungu, ya kwamba nyumba ya Mungu ni ya wote, tajiri, masikini, kabila zote maana sote tumetengenezwa kwenye mfano wa Mungu’’, alisema askofu Ochami
Naye askofu Robert Mboya alisema kuwa uteuzi wa askofu Kanyaru haukutekelezwa kwa usawa na watahakikisha aliyepokonywa nafasi hiyo anarejeshwa uongozini.
Taarifa ya Janet Mumbi.