News
Vijana Kilifi wanataka kuhusishwa kwenye mipango ya serikali
Baadhi ya vijana kaunti ya Kilifi waliohudhuria kongamano la kuadhimisha wiki ya vijana lililofanyika katika chuo cha Pwani Jumatano wameitaka serikali kuendeleza mikakati ya kuwainua vijana kiuchumi kama njia mojawapo ya kuwaimarisha.
Wakiongozwa na Mary Dama Thoya ambaye ni mjasiriamali lakini pia kijana mkaazi wa Tezo, vijana hao walisema kuwa ni jukumu la serikali kikatiba kuwezesha vijana kupitia mipango mbalimbali.
Dama alisema kuwa kupitia mipango hiyo vijana wataweza kupigwa jeki kiuchumi hali itakayopelekea ustawi wa taifa.
Kwa upande wake Peris Mbeyu Munga alieleza kusikitishwa na swala kuwa kaunti ya Kilifi haina sera maalum zinazotumika katika uongozi wa vijana baada ya kubainika kuwa ni kaunti ya Taita Taveta pekee ambayo inasera hizo katika ukanda mzima wa pwani
Naye Eddy Fondo alisema kuwa kupitia vijana kuhusishwa mara kwa mara kwenye maswala yanayowanufaisha ni wazi kuwa vijana wataweza kupata fursa mbalimbali.
Taarifa ya Hamis Kombe