News
Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma waapa kuendelea na mgomo
Shughuli za masomo katika vyuo vikuu vya umma nchini zinaendelea kuathirika huku mgomo wa kitaifa wa wahadhiri ukiingia siku ya tatu leo.
Katibu mkuu wa chama cha wadhiri katika chuo kikuu cha pwani UASU Chris Ng’eny alisema serikali imekataa kuafikia mkataba wa maelewano wa mwaka 2017/2021 ambapo wanadai serikali shilingi bilioni 5.5.
Vile vile Ng’eny alisema kuna mikataba mingine ambayo serikali walielewana, japo kufikia sasa haijatekelezwa na wataendelea kususuia masomo hadi hatua zitakapochukuliwa.
Katibu huyo akizungumza na Coco Fm Ng’eny alisema serikali imekuwa ikitumia mbinu za uongo kushawishi wahadhiri kurejea madarasani kundelea na shughuli zao, japo hilo hawatalikubali.
“Serikali inatumia uongo sana, tarehe 15, waziri wa elimu aliandika barua kwa katibu wetu mkuu Daktari Constantine Wesonga kwamba wameachilia pesa shilingi bilioni 2.50 lakini hiyo pesa hatujaiona, jana wameandika taarifa kwa vyombo vyahabari kwamba wametoa pesa yote shilingi bilioni 2.73 lakini hayo yote ni uongo, tunasubiri kuona hiyo pesa mahali iko hatujaiona ndio maana tuko kwa mgomo”,alisema Ng’eny.
Kwa upande wake mwekahazina katika chama watetezi wa wafanyikazi katika chuo kikuu cha Pwani- KUSU, Saidi Kaonge, alishinikiza serikali kutekeleza lalama za wahadhiri baada ya mazungumzo ya awali, huku akitilia shaka iwapo serikali itaitisha mazungumzo mengine.
“Tumekubaliana na hao wacha watulipe kwa awamu kwa sababu walisema kwamba hawana pesa yakutosha, awamu ya kwanza wakalipa, awamu ya pili ndio hii nataka ufahamu ya kwamba hii awamu niyamakubaliano ya mwaka 2021/25 sasa hii ni awamu ya kwanza, awamu ya pili ya malipo ya hayo makubaliano ya mwaka 2021/21 inatakiwa ilipwe mwaka ujao 2026/27 sasa wasiwasi wetu ni kwamba iwapo haya marupurupu ya awamu ya kwanza hamtulipi je hayo marupurupu yajayo tutayafuatilia kwa njia gani”, alisema Kaonge.
Mgomo huo umeathiri wanafunzi wengi nchini hasa wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo kwa mara ya kwanza.
Taarifa ya Joseph Jira